September 11, 2015

Viongozi wa Dini mbali mbali wawanyoshea vidole wanasiasa

Viongozi wa Dini mbali mbali  wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kucheza mpira wa miguu unalenga kuimarisha Amani na upendo Mkoa wa Arusha

Viongozi wa Dini  wawanyoshea vidole wanasiasa

 

Na Mary Mwita Arusha

 

VIONGOZI wa Dini mbali mbali katika Kanda ya Kaskazini wamewanyoshea vidole wanasiasa wanavuruga Amani kwa maslahi yao binafsi na kudai kuwa hawana hoja za kuwauza badala yake wanatumia muda mwingi kuchafuana majukwaani hali inayohatarisha Amani  na Upendo miongoni mwao na wananchi wanaowasikiliza .

Askofu Stanely Hotay , wa Kanisa la Angalikan Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, akizungumza katika kongamano la  wadau wa Amani  lilihusisha  dini mbali mbali , lilofanyika katika Hotel ya Golden Rose Jijini Arusha ,alisema kuwa Wanasiasa wanatakiwa kutumia lugha za kujenga na kuelezea sera zao na siyo majungu.

Hotay alisema kuwa katika hali ya kawaida unaweza kusema wamachinga ni bora kuliko baadhi ya wanasiasa kwa kuwa wanauza bidhaa zao na kuombana chenji bila kubezana

“Unajua wanasiasa , wamachinga wamewazidi, wanashangaza sana ,wanavuruga amani ya nchi yetu ,kwa kutoa lugha zenye ushawishi wa vurugu katika majukwaa ,wakati mwingine kukashifiana miongoni mwao badala ya kueleza sera ,hii ni hatari wanasiasa kama hao hawahitajiki katika jamii kwa kuwa hata kama wanakichaguliwa watakuwa ni kiini cha machafuko nchini ,na wananchi wanapaswa kuwa makini  “:alisema Hotay

Alisema kuwa ustaarabu kwa baadhi ya wanasiasa ni sifuri na kudai kusisitiza kuwa Wafanyabiashara maarufu kama wamachinga wamewapita ustaarabu ,kwa kuwa wameshuhudiwa wakiwa wanafanya kazi zo kwa nidhamu kwa kushirikiana huku wakiwa katika eneo moja ,na hata kusaidiana kuuziana bidhaa

“Mimi nisema kuwa wanasiasa wasivuruge Amani yetu ,lazima watambue kuwa Amani ikipotea hakuna kitakachoendelea ,watoto hawatakwenda shule ,wafanyakazi hawatafanya kazi hata ninyi waandishi wa habari hamtaweza kuwa huru kuandika habari zenu ,hivyo hata ninyi kuweni makini na habari zenu  epukeni uchochezi “alisisitiza Hotay

Kimsingi alisema kuwa wakati umefika  wa wanasiasa kubadilika na kueleza sera na siyo kuchafuana kama ilivyo sasa ,na kudai kuwa vitendo vinahatarisha Amani .

Kwa upande wake ,Sheikh wa Mkoa wa Arusha  anaitwa Shaban Juma alisema kuwa wanasiasa wanapaswa kuheshimiana na kuepuka uchochezi wa kisiasa unaweza kuvuruga amani ,na kusababisha machafuko katika jamii  na kudai kuwa wananchi watawachagua kwa hoja zao na siyo lugha za kashfa

Sheikh   Juma alisema kuwa ni aibu baadhi ya wanasiasa kutumia muda mwingi kutoa lugha za kashfa majukwaani badala ya kueleza sera na kusisitiza kuwa wanapaswa kueleza kwa nini wanagombea nafasi husika na siyo  kutoleana lugha za matusi.

 “Baadhi ya wanasiasa wamepoteza heshima zao ,wamesahau hata ustaarabu na utamaduni wa Mtanzania ,wa kuheshimiana ,wanatumia muda mwingi ,kutukana badala ya kueleza wananchi wakiwachagua wataondolea vifi kero zao,naomba Siasa isiharibu heshima na ustaarabu wa kuheshimiana kama waumini na Viongozi wa Dini  mbali mbali

Kinachotokea kwa sasa ni ishara ya wanasiasa kuwagawa hata waumini wa dini mbali mbali kwa maslahi yao binafsi watanzania tukatae viongozi kama hao ,na wala msiwachague kwa kuwa nia yao siyo nzuri kwa Taifa na wananchi wa Tanzania “alisema  Sheikh Juma

Anaongeza kuwa Tanzania imekuwa ni nchi ya Amani ,na kuwa hakuna sababu ya siasa chafu kupewa nafasi za kuvuruga Amani ambayo imekuwepo tangu uhuru na ambayo imeenziwa na  waasisi wa Taifa hili

“Tanzania ni nchi ya Amani ,mtakubaliana na mimi kuwa nchi  hii  kutokana na kuwa na Sifa njema ya Amani na utulivu imekuwa ni msuluhishi wa nchi zenye migogoro kupitia Viongozi wa nchi kwa hivyo ,tukatae wanasisa uchwara wasiharibu nchi yetu alisema” Sheikh Juma

Katika hatua nyingine  Viongozi hao walipongeza kamati ya Amani na Upendo ya Dini mbali mbali inayoongozwa na Mchungaji Andrew Kajembe na Katibu wa Bakwata ,Sheikh Abdalla Masood ,kwa kuandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na wadau wa Amani nchini

Alisema kuwa kongamano kama hilo linakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda Amani na kukiri kuwa bila Amani hakuna maendeleo na shughuli yeyote haiwezi kufanyika .

Kongamano hilo lilipambwa na michezo mbali mbali ,ikiwa ni pamoja mpira wa miguu ,mpira wa mkono ,kufukuza kuku,na kuvuta kamba michezo iliyochezwa na Maaskofu ,Wachungaji na Masheikh wa kanda ya Kaskazini
Mwisho…………………………………………………………………………



 

No comments:

Post a Comment