July 17, 2013

Nane Nane Kanda ya Kaskazini kufana mwaka huu

Mwenyekiti wa TASO Kanda ya Kaskazini Athur Kitonga ,wakati wa mahojiano na  blog hii




Maonesho Nane Nane Kanda ya Kaskazini  kutoa tafsiri ya Mapinduzi ya  Kilimo na Mifugo,Washiri 324 kutoka ndani na nje wadhibitisha kushiriki

Na Mary Mwita, Arusha

MAONESHO  ya Nane nane(TASO)  yanafungua milango kwa wadau wa kilimo na mifugo kubadilishana uzoefu wa shughuli zao na hatimaye kuzalisha kwa ubora  mazao yanayotokana na mifugo na kilimo.

Maonesho hayo hufanyika kila mwaka  ikiwa walengwa wakuu ni wakulima na wafugaji ,ambao wanapata fursa yakuonyesha bidhaa zao za mifugo

Kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni  Zalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga mahitaji ya soko .

Katika kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha ,Manyara na Kilimanjaro  maandalizi yamekamilika  kwa  zaidi ya asilimia 75 .

Mwenyekiti wa TASO  Kanda ya Kaskazini, Athur Kitonga anasema kuwa wadau wa maonyesho tayari wameandaa maeneo yao ya maonesho ikiwa ni pamoja na kupanda vipando vya mazao mbali mbali katika maeneo husika

Kitonga anabainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuvunja rekodi kwa kuwa tayari washiriki wa maonesho 324  wamedhibitisha kushiriki ,ikiwa ni kutoka ndani na nje ya nchi

Anataja baadhi ya washiriki kuwa ni kutoka nchi ya Kenya ,Rwanda ,Burundi  na Pakistani .

Washiriki wa ndani ni Taasisi za Serikali ,watu binafsi ,makampuni ya bidhaa za kilimo na mifugo na wadau wengine wa maendeleo ya kilimo na mifugo .

Halmashauri za Wilaya zikiwa ni wadau muhimu katika maonesho hayo ,wanatarajiwa kuandaa wakulima na wafugaji kushiriki katika maonesho hayo ,kwa kuwagharamia usafiri na malazi.

Kitonga anasema kuwa katika kuwezesha wakulima na wafugaji kujifunza mbinu bora za kilimo na mifugo mwaka huu ,wameomba kila Halmashauri ilete wakulima na wafugaji 100.

Anasema kuwa washindi bora watazawadiwa na TASO kwa kushirikiana na Halmashauri zao .

Pamoja na mambo mengine anasema kuwa wamedhamiria kuhamasisha ufugaji bora ,kuwa wafugaji watazawadiwa wakilenga wilaya mahiri kwa ufugaji wa mifugo ,ikiwa ni kuamusha ari ya kufuga mifugo kwa ubora kwa kufuata mfumo  bora wa ufugaji.

Katika kuboresha mazingira ,anasema kuwa tayari wameweza kupanda miti 1000,ikiwa ni kuwezesha kuboresha mazingira kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho

Kitonga anawaondowa wasiwasi wananchi watakaoshiriki katika maonesho hayo kuwa Usalama uko wa kutosha na kuwa kampuni ya Intellegence Securio kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wamejizatiti kuhakikisha kuwa ulinzi unakuwa imara ,na kuwa hakuna haja yakuwa na hofu yakutembelea  na kushiriki katika maonesho ya Nane Nane Mkoa wa Arusha .

Anasema kuwa Maonesho hayo yatafunguliwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini Magessa Mlongo na kufungwa na Makamu wa Rais Mohamed Bilali

Akizungumzia maendeleo ya Uwanja huo Kitonga anasema kuwa uwanja huo ,unatarajiwa kuleta maendeleo makubwa ya kilimo na mifugo ,kwa kuwa wanatarajia kujenga Hosteli kwa ajili ya wadau wa maonesho itakayowezesha kulala na kujifunza mbinu za kilimo na mifugo .

Kitonga anavunja ukimya kwa kueleza kuwa ujenzi  wa Hosteli huo unatarajiwa kuchangiwa na Serikali ikiwa watatoa Tshs million 300 ,ahadi iliyotolewa na Profesa Jumanne Maghembe wakati wa Sherehe za Nane Nane mwaka 2011 Mkoa wa Arusha .
Pia anasema kuwa wanatarajia kujenga Chuo bora cha mifugo na kilimo katika Uwanja wa Nane Nane ,Njiro Mkoa wa Arusha ,ambacho kitatoa elimu ya kilimo na mifugo ,na kuwezesha wahitimu kutumia elimu yao kusaidia jamii kufuga na kulima kwa ubora zaidi .

“Chuo hicho usajili wake uko katika hatua za mwisho ,na kwa kweli Chuo hicho kitafungua mlango kwa watu kujifunza kilimo na mifugo ,na hapa Nane nane ,itakuwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo ,lengo kuu ni kuona watu wanafanya shughuli zao kwa tija ,baada ya kupatiwa elimu “anasema Kitonga

Kitonga  anawahitimisha mahojiano na mwandishi wa Makala hii kwa kuwakaribisha wananchi kushiriki katika maonesho hayo ikiwa na kueleza kuwa maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuvunja rekodi na kuwa miundo mbinu ya uwanja imeimarishwa .

No comments:

Post a Comment