July 31, 2013

Mwanamke Happiness akombolewa na wanawake wa SIAT

Rais wa SIAT Anna Anatoli akielezea ,hali ya ukatili katika Wilaya ya Arumeru
 Ukatili wa Kijinsia Arumeru waota mizizi ,SIAT yavalia Njuga tatizo ,hilo ,Kalamu ya waandishi yanusuru baadhi ya wanawake
Mwandishi Mary Mwita ,akiwa nje ya Mwanamke  Happiness Soine aliyekumbana na Ukatili wa Kijinsia ,Kalamu ya Mary Mwita ,imesaidia mwanamke huyo kukombolewa na kujengewa nyumba na wasamaria wa SIAT

Na Mary  Mwita ,Arusha

Vitendo vya Ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake hapa nchini kwa miaka ya hivi karibuni vimepungua kutokana na jitihada za wadau wa kutetea haki za binadamu kuvalia njuga tatizo hilo ,kwa kuwachukulia hatua wahusika .

Wanawake katika  baadhi ya jamii wameonekana hawana haki ,na hivyo kunyanyaswa  na hata kunyanganywa mali  walizochuma na wanaume zao ambao wametangulia mbele ya haki .

Katika Wilaya ya Arumeru ,ukatili dhidi ya wanawake ,umejikita katika baadhi ya jamii,wanawake wakinyanyaswa  na hata kufukuzwa katika nyumba walizojenga na wanaume zao .

Mfano halisi ni wa mwanamke Happiness  Soine aliwahi kuandikwa katika gazeti la Mtanzania mwaka 2010 kuwa alikuwa ananyanyaswa na  shemeji yake ,ambaye alidaiwa kumiga na kumjeruhi katika sehemu nyeti .

Wadau wa maendeleo baada ya kusoma habari hiyo ,iliyokuwa imeandikwa na Bi Mary Mwita ,walivyalia njuga tatizo hilo ,na kufanikiwa kufika kijijini kwa Happiness katika Kata ya Kingori ,Wilaya ya Arumeru .

Umoja wa wanawake wanataaluma unaoujulikana kama   SIAT(Soroptimist  International  Arusha  Tanzania) ,yenye Makao Makuu Mkoa wa Arusha  ndiyo walioguswa na mkasa wa Happiness na kulazimika kuwachukulia hatua wahusika na mwanamke huyo kuwa huru .

Wanawake hao wakiongozwa na Rais wa Umoja huo ,Anna  Anatoli walifanikiwa   kushughulikia kesi feki zilizokuwa zimefunguliwa kumkadamiza  Bi Happiness,kuwafikisha mahakamani watuhumiwa  na kumjengea nyumba ambayo imezinduliwa na Katibu Tarafa  katika Halmashauri ya Meru ,Bwana Sumari aliyemwakilisha  Mkuu wa Wilaya ya Arumeru  .

Rais Anatoli akitoa simulizi ya mkasa wa Happiness anasema kuwa ipo haja ya wadau wa haki za binadamu kuendelea  kusaidia jamii husani wanawake wanaokadamizwa na kunyimwa haki katika jamii wanazoishi .

Anapongeza waandishi wa habari kwa kutumia kalamu zao vyema kumwulika maovu na kuyaanika katika jamii ,na kueleza kuwa kama isingekuwa ni kalamu ya Mary Mwita wasingeweza kujua taabu na mateso aliyokuwa anapata mwanamke huyo .

Anafafanua kuwa umoja na Shirika lao ,nilakujitolea ,hawana wafadhili ,wanajitolea kujichangisha kama wanawake wanataaluma mbali mbali ,ikiwa  lengo lao ni kuona kuwa  wanawake wenzao wanaishi kwa amani na furaha  na kusaidia familia zao

Ana Anatoli  anasema kuwa pia wameweza kusaidia wasichana zaidi ya 100 waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ngono kabla ya wakati na kuwa waliobainika kuathirika na vitendo hivyo wanaendelea kuangaliwa kwa ukaribu ,ikiwa ni kuwawezesha kurudi na kuishi maisha ya kawaida na kujishughulisha kiuchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Munasa Nyerembe katika taarifa yake iliyosomwa na Katibu Tarafa Bw,Sumari anasema kuwa ,Serikali   kwa kushirikiana na wadau wa Haki za Binadamu itaendelea itaendelea kuhakikisha kuwa makundi yote katika jamii yanaishi kwa amani na kutendewa haki  na kuwaajibisha wanaowanyanyasa .

Nyerembe anapongeza wanawake hao na kuwataka kuendelea kusaidia makundi zaidi katika jamii ,na kueleza kuwa Serikali inatambua mchango wa wao na kuwa Serikali haiwezi kutekeleza majukumu  pekee yao bila kupata msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama SIAT

Mkuu huyo pia anachukua fursa hiyo kupongeza jitihada za Mwandishi Mary Mwita zakuandika habari za kweli ,na kuwezesha wahusika kuchukua hatua stahiki kama alivyofanikisha habari ya Mwanamke Happiness kufikia umma wa Watanzania na kujitokeza kumsaidia na kumjengea Nyumba .

Aidha anasema Serikali haitawaonea haya  watu wanaonyanyasa wanawake na kueleza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia tatizo la Happiness ,ikiwa ni kuhakikisha kuwa anaishi kwa amani ,na kukomesha ukatili dhidi yake na mashemeji zake ,ambao wanataka kumyanganya mali alizochuma na mume wake.

Halmashauri ya Meru ,ni miongoni mwa Halmashauri hapa nchini ambazo ukatili dhidi ya wanawake umejikita ,ni jukumu la wadau kuvalia njuga tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment