July 31, 2013

Mwanamke Happiness akombolewa na wanawake wa SIAT

Rais wa SIAT Anna Anatoli akielezea ,hali ya ukatili katika Wilaya ya Arumeru
 Ukatili wa Kijinsia Arumeru waota mizizi ,SIAT yavalia Njuga tatizo ,hilo ,Kalamu ya waandishi yanusuru baadhi ya wanawake
Mwandishi Mary Mwita ,akiwa nje ya Mwanamke  Happiness Soine aliyekumbana na Ukatili wa Kijinsia ,Kalamu ya Mary Mwita ,imesaidia mwanamke huyo kukombolewa na kujengewa nyumba na wasamaria wa SIAT

Na Mary  Mwita ,Arusha

Vitendo vya Ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake hapa nchini kwa miaka ya hivi karibuni vimepungua kutokana na jitihada za wadau wa kutetea haki za binadamu kuvalia njuga tatizo hilo ,kwa kuwachukulia hatua wahusika .

Wanawake katika  baadhi ya jamii wameonekana hawana haki ,na hivyo kunyanyaswa  na hata kunyanganywa mali  walizochuma na wanaume zao ambao wametangulia mbele ya haki .

Katika Wilaya ya Arumeru ,ukatili dhidi ya wanawake ,umejikita katika baadhi ya jamii,wanawake wakinyanyaswa  na hata kufukuzwa katika nyumba walizojenga na wanaume zao .

Mfano halisi ni wa mwanamke Happiness  Soine aliwahi kuandikwa katika gazeti la Mtanzania mwaka 2010 kuwa alikuwa ananyanyaswa na  shemeji yake ,ambaye alidaiwa kumiga na kumjeruhi katika sehemu nyeti .

Wadau wa maendeleo baada ya kusoma habari hiyo ,iliyokuwa imeandikwa na Bi Mary Mwita ,walivyalia njuga tatizo hilo ,na kufanikiwa kufika kijijini kwa Happiness katika Kata ya Kingori ,Wilaya ya Arumeru .

Umoja wa wanawake wanataaluma unaoujulikana kama   SIAT(Soroptimist  International  Arusha  Tanzania) ,yenye Makao Makuu Mkoa wa Arusha  ndiyo walioguswa na mkasa wa Happiness na kulazimika kuwachukulia hatua wahusika na mwanamke huyo kuwa huru .

Wanawake hao wakiongozwa na Rais wa Umoja huo ,Anna  Anatoli walifanikiwa   kushughulikia kesi feki zilizokuwa zimefunguliwa kumkadamiza  Bi Happiness,kuwafikisha mahakamani watuhumiwa  na kumjengea nyumba ambayo imezinduliwa na Katibu Tarafa  katika Halmashauri ya Meru ,Bwana Sumari aliyemwakilisha  Mkuu wa Wilaya ya Arumeru  .

Rais Anatoli akitoa simulizi ya mkasa wa Happiness anasema kuwa ipo haja ya wadau wa haki za binadamu kuendelea  kusaidia jamii husani wanawake wanaokadamizwa na kunyimwa haki katika jamii wanazoishi .

Anapongeza waandishi wa habari kwa kutumia kalamu zao vyema kumwulika maovu na kuyaanika katika jamii ,na kueleza kuwa kama isingekuwa ni kalamu ya Mary Mwita wasingeweza kujua taabu na mateso aliyokuwa anapata mwanamke huyo .

Anafafanua kuwa umoja na Shirika lao ,nilakujitolea ,hawana wafadhili ,wanajitolea kujichangisha kama wanawake wanataaluma mbali mbali ,ikiwa  lengo lao ni kuona kuwa  wanawake wenzao wanaishi kwa amani na furaha  na kusaidia familia zao

Ana Anatoli  anasema kuwa pia wameweza kusaidia wasichana zaidi ya 100 waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ngono kabla ya wakati na kuwa waliobainika kuathirika na vitendo hivyo wanaendelea kuangaliwa kwa ukaribu ,ikiwa ni kuwawezesha kurudi na kuishi maisha ya kawaida na kujishughulisha kiuchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Munasa Nyerembe katika taarifa yake iliyosomwa na Katibu Tarafa Bw,Sumari anasema kuwa ,Serikali   kwa kushirikiana na wadau wa Haki za Binadamu itaendelea itaendelea kuhakikisha kuwa makundi yote katika jamii yanaishi kwa amani na kutendewa haki  na kuwaajibisha wanaowanyanyasa .

Nyerembe anapongeza wanawake hao na kuwataka kuendelea kusaidia makundi zaidi katika jamii ,na kueleza kuwa Serikali inatambua mchango wa wao na kuwa Serikali haiwezi kutekeleza majukumu  pekee yao bila kupata msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo kama SIAT

Mkuu huyo pia anachukua fursa hiyo kupongeza jitihada za Mwandishi Mary Mwita zakuandika habari za kweli ,na kuwezesha wahusika kuchukua hatua stahiki kama alivyofanikisha habari ya Mwanamke Happiness kufikia umma wa Watanzania na kujitokeza kumsaidia na kumjengea Nyumba .

Aidha anasema Serikali haitawaonea haya  watu wanaonyanyasa wanawake na kueleza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia tatizo la Happiness ,ikiwa ni kuhakikisha kuwa anaishi kwa amani ,na kukomesha ukatili dhidi yake na mashemeji zake ,ambao wanataka kumyanganya mali alizochuma na mume wake.

Halmashauri ya Meru ,ni miongoni mwa Halmashauri hapa nchini ambazo ukatili dhidi ya wanawake umejikita ,ni jukumu la wadau kuvalia njuga tatizo hilo.

July 17, 2013

Nane Nane Kanda ya Kaskazini kufana mwaka huu

Mwenyekiti wa TASO Kanda ya Kaskazini Athur Kitonga ,wakati wa mahojiano na  blog hii




Maonesho Nane Nane Kanda ya Kaskazini  kutoa tafsiri ya Mapinduzi ya  Kilimo na Mifugo,Washiri 324 kutoka ndani na nje wadhibitisha kushiriki

Na Mary Mwita, Arusha

MAONESHO  ya Nane nane(TASO)  yanafungua milango kwa wadau wa kilimo na mifugo kubadilishana uzoefu wa shughuli zao na hatimaye kuzalisha kwa ubora  mazao yanayotokana na mifugo na kilimo.

Maonesho hayo hufanyika kila mwaka  ikiwa walengwa wakuu ni wakulima na wafugaji ,ambao wanapata fursa yakuonyesha bidhaa zao za mifugo

Kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni  Zalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga mahitaji ya soko .

Katika kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha ,Manyara na Kilimanjaro  maandalizi yamekamilika  kwa  zaidi ya asilimia 75 .

Mwenyekiti wa TASO  Kanda ya Kaskazini, Athur Kitonga anasema kuwa wadau wa maonyesho tayari wameandaa maeneo yao ya maonesho ikiwa ni pamoja na kupanda vipando vya mazao mbali mbali katika maeneo husika

Kitonga anabainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuvunja rekodi kwa kuwa tayari washiriki wa maonesho 324  wamedhibitisha kushiriki ,ikiwa ni kutoka ndani na nje ya nchi

Anataja baadhi ya washiriki kuwa ni kutoka nchi ya Kenya ,Rwanda ,Burundi  na Pakistani .

Washiriki wa ndani ni Taasisi za Serikali ,watu binafsi ,makampuni ya bidhaa za kilimo na mifugo na wadau wengine wa maendeleo ya kilimo na mifugo .

Halmashauri za Wilaya zikiwa ni wadau muhimu katika maonesho hayo ,wanatarajiwa kuandaa wakulima na wafugaji kushiriki katika maonesho hayo ,kwa kuwagharamia usafiri na malazi.

Kitonga anasema kuwa katika kuwezesha wakulima na wafugaji kujifunza mbinu bora za kilimo na mifugo mwaka huu ,wameomba kila Halmashauri ilete wakulima na wafugaji 100.

Anasema kuwa washindi bora watazawadiwa na TASO kwa kushirikiana na Halmashauri zao .

Pamoja na mambo mengine anasema kuwa wamedhamiria kuhamasisha ufugaji bora ,kuwa wafugaji watazawadiwa wakilenga wilaya mahiri kwa ufugaji wa mifugo ,ikiwa ni kuamusha ari ya kufuga mifugo kwa ubora kwa kufuata mfumo  bora wa ufugaji.

Katika kuboresha mazingira ,anasema kuwa tayari wameweza kupanda miti 1000,ikiwa ni kuwezesha kuboresha mazingira kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho

Kitonga anawaondowa wasiwasi wananchi watakaoshiriki katika maonesho hayo kuwa Usalama uko wa kutosha na kuwa kampuni ya Intellegence Securio kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wamejizatiti kuhakikisha kuwa ulinzi unakuwa imara ,na kuwa hakuna haja yakuwa na hofu yakutembelea  na kushiriki katika maonesho ya Nane Nane Mkoa wa Arusha .

Anasema kuwa Maonesho hayo yatafunguliwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini Magessa Mlongo na kufungwa na Makamu wa Rais Mohamed Bilali

Akizungumzia maendeleo ya Uwanja huo Kitonga anasema kuwa uwanja huo ,unatarajiwa kuleta maendeleo makubwa ya kilimo na mifugo ,kwa kuwa wanatarajia kujenga Hosteli kwa ajili ya wadau wa maonesho itakayowezesha kulala na kujifunza mbinu za kilimo na mifugo .

Kitonga anavunja ukimya kwa kueleza kuwa ujenzi  wa Hosteli huo unatarajiwa kuchangiwa na Serikali ikiwa watatoa Tshs million 300 ,ahadi iliyotolewa na Profesa Jumanne Maghembe wakati wa Sherehe za Nane Nane mwaka 2011 Mkoa wa Arusha .
Pia anasema kuwa wanatarajia kujenga Chuo bora cha mifugo na kilimo katika Uwanja wa Nane Nane ,Njiro Mkoa wa Arusha ,ambacho kitatoa elimu ya kilimo na mifugo ,na kuwezesha wahitimu kutumia elimu yao kusaidia jamii kufuga na kulima kwa ubora zaidi .

“Chuo hicho usajili wake uko katika hatua za mwisho ,na kwa kweli Chuo hicho kitafungua mlango kwa watu kujifunza kilimo na mifugo ,na hapa Nane nane ,itakuwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo ,lengo kuu ni kuona watu wanafanya shughuli zao kwa tija ,baada ya kupatiwa elimu “anasema Kitonga

Kitonga  anawahitimisha mahojiano na mwandishi wa Makala hii kwa kuwakaribisha wananchi kushiriki katika maonesho hayo ikiwa na kueleza kuwa maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuvunja rekodi na kuwa miundo mbinu ya uwanja imeimarishwa .

July 3, 2013

Wananchi Kiteto wasifu TASAF ,wataka wadau wengine kuiga mfano wa TASAF ,kwa kushirikisha wananchi kupanga na kusimamia wenyewe miradi husika

Mwandishi Mary Mwita ,akiwa Kiteto Manyara kihoji wananchi jinsi walivyonufaika na TASAF,wadai wamenufaika kwa kupata barabara ya uhakika walioichimba na kuitengeneza wenyewe ,wataka miradi mingine ya maendeleo ifuate nyayo za TASAF,kwa kuwa inashirikisha wananchi katika kila hatua ,na hivyo imeweza kufanikiwa kutokana na ushiriki wa wananchi ,na hivyo kuondoa mianya ya wanaofuja fedha za miradi

Wasomi wa Chuo Kikuu Makumira wanaochukua Shahada ya Muziki wakicheza ngoma ya Kimasai

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Tumaini Makumira Usa River Arusha  ,wakicheza ngoma ya Kimasai ikiwa ni sehemu ya masomo yao ya Muziki

Yatima wavishwa viatu na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,ashauri jamii kuendelea kuwasaidia Yatima na makundi yenye uhitaji

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nyerembe Munasa akiwavisha watoto Yatima viatu ,ikiwa ni msaada ulitolewa na Shirika la wasabato linalojulikana kama ADRA tukio lilofanyika katika kata ya Maji ya Chai ,Wilaya ya Arumeru .