March 11, 2014

Matokeo Makubwa sasa kwenda na Ajira za Watendaji

Matokeo Makubwa sasa kugharimu ajira za Watendaji ,Mulongo aapa kuwachukulia hatua watendaji wabovu

Na Mary Mwita,Arusha .

NI jambo la kawaida kuona viongozi wakuu wa Serikali kuzuru miradi ya maendeleo na wakati mwingine kukemea na kutoa ushauri wa jinsi ya kutekeleza miradi hiyo hatimaye kunufaisha walengwa ambao ni wananchi wa maeneo husika .

Baadhi ya watendaji wanapata wakati mgumu wakati  miradi hiyo ikitembelewa kutokana na miradi husika kufanya kwa kiwango cha chini ,na hivyo kuzua mjadala na misuguano baina ya mamlaka husika

Jukumu la kuhakikisha miradi inatekelezwa katika kiwango kinachokubalika ni la kila mdau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na wananchi  wa maeneo husika .

Mpango wa Matokeo makubwa sasa (BIG RESULT NOW) kwa sasa ndiyo unawafanya viongozi wa Serikali kukuna vichwa ,kwa kuangalia miradi ambao imewekwa katika mpango huo inatekelezwa na hatimaye kuharakisha maendeleo .

Miongoni mwa Viongozi hao ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mlongo ambaye anasema kuwa ikiwa viongozi na watendaji wa Halmashauri za Wilaya Mkoa wa Arusha watashindwa kuwajibika na kuhakikisha kuwa vipaumbele kama vile Maji ,Elimu ,Mapato ,Kilimo Nishati  inafanikiwa kwa kiwango kikubwa ,atakuwa wakanza kuwachukulia hatua kabla ya yeye kuchukuliwa hatua

Mlongo anasema kuwa Viongozi wanapaswa kuwa mfano katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kuandaa mashamba ya mfano  katika makazi yao ili wananchi wajifunze kutoka kwao .

Mkuu huyo anasema kuwa baadhi ya viongozi  ni wavivu ,na hivyo kuwafanya wananchi kushindwa kujifunza mema kutoka kwao,kitendo alichodai kuwa hakiwezi kuvumiliwa hata kidogo.

“Niseme lazima tuwe mfano bora ,wa kuigwa tuwaongoze wananchi kufikia malengo ya mafanikio ,mfano suala la kilimo katika maeneo mbali mbali hapa Arumeru wananchi kila mwaka wanakosa mvua ,wanalima mahindi ,ifike mahali wahimizwe kulima mazao yanayostahimili ukame ,kama vile mtama na mihogo ,waache kungangania zao moja.”anasema Mlongo

Mlongo anasema kuwa wananchi wanahitaji kuona mabadiliko ya maisha yao ,na kuwa wataweza kuwa na maisha bora ikiwa wataongozwa kufanya shughuli zenye manufaa zitakazo waingizia kipato na kuongeza pato la familia yao .


 “Watendaji wa Halmashauri   kwa kushirikiana na madiwani wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wananchi  wanapata maendeleo   kupitia vyanzo mbali mbali vya mapato ya ndani na nje ya Halmashauri hiyo .

 Mlongo katika ziara zake  alipiga hodi katika Halmashauri ya Arusha  na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa Halmashauri hiyo ,kuhusu Matokeo makubwa Sasa                                                                                                                                                                                                        
Mkuu huyo anawataka watendaji hao kujipanga kuhakikisha kuwa wanashirikiana na wananchi kuboresha sekta hizo ikiwa ni njia yakuharakisha maendeleo na kuwapunguzia wananchi umaskini kwa kuwaondolea kero sugu .

Mkuu huyo akiwa katika Halmashauri hiyo anapata fursa ya kuzindua gari lilonunuliwa na Halmashauri hiyo kutokana na mapato ya ndani maalum kwa ajili ya idara ya elimu .

Mkuu huyo anataka gari hilo litumike kufuatilia maendeleo ya elimu katika Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kufuatilia mahudhurio ya wanafunzi na walimu katika Halmashauri hiyo .

Mara baada ya kufanya mazungumzo na watalaam hao anazuru miradi ya maji katika Halmashauri hiyo katika baadhi ya kata na kufanya mazungumzo na wakandarasi aliowakuta katika miradi maji 

Mlongo anapata ufafanuzi wa miradi hiyo kutoka kwa Mhandisi wa maji Bi Bahati ambaye anatoa ufafanuzi wa jinsi miradi hiyo inatekelezwa .

Aidha ziara hiyo inapambwa na viongozi wa Halmashauri ya Arusha ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mnasa Nyerembe ,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ,Saimon Saningo ,na Makamu Mwenyekiti Anna Msuya na watendaji wengine wa Halmashauri

Mkuu huyo anaeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kutaka wakandarasi hao kumaliza miradi hiyo kwa wakati ikiwa ni kuwaondolea wananchi kero ya kusaka maji .

Mlongo anawaonya viongozi wanaokwamisha miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Arusha kudai kuwa hatasita kuwachukulia hatua za kisheria

Mlongo anasema kuwa viongozi kama hao hawahitajiki katika jamii ya watu wastaarabu wanaowatakia wananchi maendeleo .
Hata hivyo Watendaji wa Halmashauri hiyo wanafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo na kuupa umaskini kisogo 
Katika kutekela kwa vitendo  Baraza  la Madiwani wa Halmashauri ya hiyo   limepitisha bajeti ya Tshs.37,319,148,736 ikiwa ni fedha zinazotarajiwa kupatikana katika vyanzo mbali mbali vya mapato ya ndani na nje ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Fidelist Lumato iliyosomwa na ,bajeti hiyo  ni ya mwaka fedha 2014-2015.
 Lumato analiambia Baraza la madiwani kuwa fedha hizo zitapatikana katika mchanganuo wa mapato ya Halmashauri  billion 2,707,659,500,Ruzuku ya  fidia ya mapato   431,083,000,ruzuku ya mishahara  Tshs 27,255,089,820  ,ruzuku ya matumizi mengineyo Tshs.2,720,568,000, na miradi ya maendeleo na wafadhili Tshs 4,734,884,416  .
 Anafafanua kuwa Halmashauri hiyo inakisia kutumia Tshs.37,849,293,736 ikiwa ni matumizi ya mishahara ,matumizi mengineyo ,michango ya Halmashauri katika miradi mbali mbali ya maendeleo ,ruzuku ya mishahara ,matumizi mengineyo ya Ruzuku ,miradi ya maendeleo na ruzuku .
 Bwana , Lumato anasema  kuwa kutokana na ukomo wa bajeti hiyo Halmashauri imelazimika kuleta maombi maalum kwa ajili ya miradi ya vijiji 19ikiwa ni kiasi cha Tshs Billion 5,455,978,106.36

Miradi mingine iliyoombewa fedha ni mradi wa ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) Hospitali ya Wilaya Tshs 1,800,000,000, ujenzi wa Sekondari  Tshs.200,000,000 ,Ujenzi wa Hostel za Sekondari –maeneo ya wafugaji Tshs.200,000,000,

Nyingine ni ukamilishaji wa Jengo la Halmashauri Tshs.200,000,000 ,ujenzi wa Vivuko Tshs .800,000,000 ,ujenzi wa Bwawa la kukinga maji mafuriko Tarafa ya Mukulat,pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa maeneo

Baraza hilo lilipitisha Bajeti hilo kwa sauti ya pamoja na kutaka watendaji kutekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo na kufuatilia mapato ,ikiwa ni kuwezesha Halmashauri hiyo kupata mapato kwa wakati na kutekeleza miradi ya maendeleo .
 Mwisho………………………………………

Magessa Mulongo alia na Big Result Now

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulongo wakati wa Ziara ya kukagua Miradi Meru ya BIG Result Now

Vijana Angalikan Tanzania wasema wamechoka na kutumiwa vibaya na wenye Fedha wajipanga kuinua uchumi wao


Vijana Angalikan Tanzania wasema kutumiwa na Wenye Fedha basi wajipanga kujiinua kiuchumi


Na Mary Mwita Arusha.

VIJANA wanatajwa kuwa ndiyo wenye nguvu ,na ambao wanaweza kuleta mapinduzi ya maendeleo  katika jamii na Taifa kwa ujumla .

Huo ni ukweli usiopingwa  na mtu yeyote ,lakini mtihani na swali ni kuwa ni wapi vijana wapate fursa yakuonyesha uwezo wao ikiwa hawana kipato hata cha kuanzisha mradi wa kuku ama mahindi .

Vijana walio wengi hawana ajira ingawa wamesoma ,na wengine hawana kipato cha kuanzisha miradi ,jambo linalowakatisha tamaa na kulazimika kujiingiza katika vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na uvutaji bangi .

Tatizo la vijana linapaswa  kupewa msukumo wa pekee wa maendeleo   kwa kuwahamasisha kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili kuepuka kuwa tegemezi katika jamii wanazoishi .

Ni wazi kuwa migogoro mingi ya kisiasa inaongozwa na vijana kwa kutumiwa na watu wenye nguvu ya fedha kwa kuwapatia hongo ya pombe na sigara,ili waweze kukabiliana na maadui wa Siasa .

Ikiwa jamii  na Taifa inapenda kuona hatima ya vijana ikiwa njema ni vyema ikiwasaidia kuwapatia elimu bora ya ujasirimali 

Hata hivyo ,Tayari hata Kanisa limeona kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni kikwazo kwa vijana ,hata makanisani na kuwafanya kutumiwa na viongozi wa Dini wasiokuwa na Hofu ya Mungu .

Vijana wa Kanisa Angalikani Tanzania yaani Jimbo ,wameona athari ya kutumiwa na wenye fedha ,na wameeleza bayana kuwa Vijana wametumiwa katika uchaguzi wa Maaskofu ,kwa kuhakikisha kuwa Askofu anayechaguliwa ni matakwa ya  kundi fulani .

Katika kuondoa hali hiyo wanasaka dawa ya  Muarubaini ambao wamedai kuwa ni kuimarisha uchumi wa Vijana kwa kuwahimiza kushiriki katika miradi ya maendeleo ,pamoja na kuanzisha miradi ya uzalishaji itakayokuwa na manufaa ya haraka na kwa kundi kubwa .

Mwenyekiti wa Vijana Angalikani Jimbo  Jonson Mgimba Tanzania anasema kuwa katika kufanikisha malengo yao wanatajia kuboresha Katiba ya Umoja wa Vijana wa Angalikan Tanzania ,ili kuweza kuweka mambo muhimu ambao hayapo kwa ajili ya Vijana ikiwa ni pamoja na kamati za  miradi .
Kimsingi anajigamba kuwa Vijana wanaweza na kuwa wakati wakutumiwa na wenye fedha makanisani  na Serikalini imekwisha ,kwa kuwa wamekuwa daraja la mafanikio ya watu wenye  uwezo wa fedha ,na baada ya kufanikiwa wanapewa kisogo .

Naomba kuuliza Hivi ni kweli hatuwezi kweli ?Ni jibu rahisi sana ,tunaweza ,tunatakiwa kujiamini ,na tunaweza kufanikiwa kiuchumi kupitia njia mbali mbali na zipo ,hivyo tujipange na tushirikiane kwa pamoja ,huku tukiomba wadau wenye mapenzi mema kujitokeza kutusaidia .

Mwenyekiti huyo anaeleza kuwa ipo miradi Lukuki ya Maendeleo  ambayo vijana wakiwezeshwa  watafanya na kuepuka kuwa tegemezi .

“Niwambie Vijana wenzangu sisi tunazonguvu ,hakuna jambo tunaloweza kushindwa ikiwa tutaamua kufanya na kujituma ,na Maandiko Matakatifu yanatamka bayana umuhimu wa Vijana ,Biblia inamuulezea Kijana ni nani ,hivyo tuamue kwa vitendo na tuonyeshe jamii kuwa tunaweza .”anasema

Katika kuonyesha kwa vitendo Vijana hao wanalazimika kuanzisha mchango baina yao na wadau waliohudhuria mkutano huo ,na kuweza kupata zaidi ya Million 15 ikiwa ni ahadi na fedha taslimu .

Vijana hao wakiwa katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Morogoro yaani (WAMO) wanaeleza furaha yao kwa mgeni Rasmi katika mkutano wao wa siku Mbili ,Askofu Stanely Hotay wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro kuwa ,wanajiona wenye faraja wakiona viongozi wao wakiwaunga mkono .

Wanashindwa kuficha furaha yao na kueleza kuwa Askofu huyo amekuwa karibu na vijana wa Kanisa hilo ,na kuomba awe Mshauri wao wa karibu kwa kuwa wameona kuwa ana nia dhabiti na Vijana.

Aidha wanamtaja mtu mwingine kuwa ni Bwana Mgaya ,ambaye wanadai ni mtumishi wa Mungu ambaye ameona umuhimu wa Vijana na kuwasaidia pindi walivyohitaji msaada wake.

Katika hatua nyingine wanamshukuru Askofu Mkuu wa Kanisa hilo na Katibu Mkuu wa Kanisa hilo kwa kushiriki katika mkutano wa Vijana na kuzungumza nao ,na kueleza kuwa wamepata nguvu ya kuendeleza mikakati ya kujikomboa katika umaskini .

“Tunashukuru kwa michango na ushauri wenu tunaendea kufanyia kazi ,tunaomba msichoke kutusaidia ,tunahitaji msaada wenu kama walezi ,na marafiki wa kweli wa Vijana “.anasema


Kwa upande wake Askofu Stanely Hotay hakusita kuzungumza na Vijana hao kuhusu kupinga maovu ,hususuani suala la ushoga ,ambalo Mataifa ya Magharibi wamelivalia Nguja .

Hotay anasema kuwa amekuwa  ni miongoni wa Viongozi waliohudhuria mkutano wa kupinga Ushoga na alipinga bila woga na kuvutia baadhi ya Viongozi wa Nchi za Ulaya ,na kutamani kuzuru Tanzania ,kwa kuwa alionyesha msimamo kuwa hiyo ni dhambi na haina uhalali wowote.


Vijana muwe tayari kukataa maovu ,na maovu mukatae wakati wowote mchana na usiku ,lazima Mungu aheshimiwe na ninyi vijana munayo nafasi kubwa sana kupinga kila jambo baya ,msikubali kutumiwa na watu waovu waliokata tama ,bali kuweni kielelezo cha kuonyesha watu njia sahihi .

“Maisha na mazingira magumu yasiwafanye mukashiriki katika maovu ,Mataifa ya Magharibi yanatuburuza kwa kutaka tufanye matakwa yake msikubali hata kidogo ,lazima mujue kuwa mpango wao wa kuhimiza ushoga hakuuanza leo ,walionzisha mpango huo wamechukua muda mwingi na hata kuingia Vyuoni na kufundisha vijana watakaofanikisha malengo yao ,hivyo kuweni makini sana ,kwa kuwa Mungu wetu hadhihakiwi “

Ni wazi kuwa hao wanaohimiza ushoga hawakuanza leo ni mkakati wa muda mrefu wa kutenda dhambi ,walianza miaka 30 iliyopita ,na wamefanyta hivyo katika vyuo vikuu katika nchi husika kufundisha vijana miaka 3 ,ikiwa ni kuwaandaa kuhimiza ushoga na huo ni mradi wao ,hivyo vijana kuweni macho .

Askofu Hotay akiwa ananukuu maandiko Matakatifu katika Biblia kitabu cha Warumi 10 anawataka Vijana kuwa mstari wa mbele kupinga maovu

Vijana nawataka dhambi muitangaze mchana na wala siyo usiku ,yaani msione haya  kutangaza dhambi ili wanaotenda waache na kumfuata Mungu .
Hotay anaendelea kuwapa kiburi vijana kuwa wana nguvu na mtu awaye yote asiudharau ujana wao ,huku akinukuu maandiko matakatifu ITimotheo 12;6

Pamoja na mambo mengine anakemea ushirikina na kudai kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika inayoongoza kwa Ushirikina ,na kuwataka vijana kuepuka ushirikina kwa kuwa Mungu  ni zaidi ya yote ,kwa kuwa hata hao washirikiana wanataja Mungu ,japo hawajui ni Mungu yupi wanayemwabudu.

Askofu huyo pia anasisitiza kuwa wote waliondoka katika Imani ya kweli  wanazo njia zao wanazofuata na kutaka vijana kusimama katika Imani na kumwamini Mungu wa kweli ,na kunukuu maandiko Matakatifu katika Biblia katika ITimotheo 1-4 kuwa kila anayeacha imani ya kweli afuata njia zake.

Naye Askofu Mkuu wa Tanzania ,alizungumza na Vijana hao nakuwataka kuanza sasa kujitegemea kwa kuwa ameona  nia yao njema ya kujikomboa ,na kudai kuwa Kanisa linawaunga mkono na kuwataka kuanza mchakato wa kurekebisha Katiba mapema ,ili mabadiliko ya kiuchumi na mambo mengine ya Msingi yaweke kwenye Katiba .

Askofu huyo kwa kuunga jitihada za Vijana mkono anaahidi kuchangia Milion 3 kwa ajili ya mfuko wa jimbo Vijana ,na kuungwa Mkono na Askofu Hotay anayechangia million 1.

Mwenyekiti wa Vijana Jimbo Angalikan Tanzania ,atoa angalizo kwa Vijana kuwaepuka wenye Fedha

Mwenyekiti wa Vijana Jimbo Angalikani Tanzania ,Jonson Mgimba akitoa hotuba Vijana wa Angalikan Tanzania,WAMO Morogoro

Ukatili watikisa Arumeru,Wanawake waapa kukabiliana nao

Ukatili wa  Wanawake Arumeru bado ni Tatizo ,Siku ya wanawake yaazimishwa kwa majonzi


Na Mary Mwita ,Arumeru.

SUALA la Ukatili wa Wanawake katika Jamii mbali mbali hapa nchini bado ni tatizo ikiwa wadau wa haki za Binadamu ,wanapigia kelele ukatili huo.

Wilaya ya Arumeru tatizo la Ukatili wa wanawake bado nikubwa ,wanawake wananyanyaswa na wanaume zao ,wanabebeshwa jukumu la kulea familia ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto .

Baadhi ya wanawake wanapiga na kujeruhiwa na wanaume zao ,lakini wanashindwa kueleza ukweli kwa vyombo vya usalama kwa kuogopa kuwajibishwa na jamii zao ikiwa watawashitaki wanaume zao .

Ingawa Siku ya wanawake  iliyofanyika tarehe 8 Machi 2014 ilifana katika maeneo mengi nchini ,lakini Arumeru hali ilikuwa yakusikitisha baada ya kupata simulizi ya jinsi wanawake wanavyofanyiwa ukatili ,huku waathirika wa matukio wakieleza mikasa iliyowapata .

Katika kata ya Oltruto ,tarafa ya Enaboishu,Halmashauri ya Arusha ,Wilaya ya Arumeru ,wanawake waliangua kilio wakati mwanamke mwenzao alivyoeleza jinsi alivyonyanyaswa na mume wake na kutelekezwa na watoto wawili .

Mwanamke huyo aliyetambulishwa kwa jina la Magreth Namnyaki ,aliwafanya wanawake wenzake wachange fedha kwa ajili ya  kumsaidia mwanamke huyo .

Mgeni Rasmi katika maadhimisho wanawake katika Halmashauri ya Arusha ,Anna Msuya ambaye ni makamu Mwenyekiti wa Halmashuri ya Arusha ,anashindwa kujizuia na kueleza hali waliyomkuta mwanamke huyo akiwa nayo .

Msuya anasema kuwa ,mwanamke huyo aliungua mikono ,na kulazwa katika Hospitali ya Selian ,na alikuwa amezuiwa na Hospitali baada ya kupona ili aweze kulipa deni la Million 13 alizotumia akiwa Hospitali hiyo .

“Jamani ukisikia unyama ,huyo Magreth amefanyiwa unyama ,fikiria kaungua akiwa na kwa mume wake ,Mume alivyoona kaungua ,kamtelekeza hadi watoto ,ambao ilibidi wapelekwe kwa nyumbani kwa mwaname hii ni hatari sana”anasema Anna Msuya

Msuya anasema kuwa Serikali ilifanya jitihada za kumsaka mwanaume huyo ,ili akamatwe ,lakini alitoroka ,na hadi sasa hajapatikana na kueleza kuwa akipatikana lazima atachukuliwa hatua ,kwa kumnnyanyasa ,mwanamke huyo .

Katika kuonyesha kuwa ameguswa na mkasa huyo Msuya anaongoza wanawake waliohudhuria maadhimisho hayo kumchangia fedha  Bi Magreth ,ili ziweze kumsaidia kununulia watoto wake chakula .

Anamchangia kiasi cha Tshs  400,000  na  wanawake wa jamii ya wafugaji wanafanikiwa kumchangia  Tshs 170,000

Bi Msuya anashukuru kwa mchango ,wa akina mama kwa mwanamke mwenzao ,na kueleza kuwa atahakikisha mwanamke huyo anaanzisha biashara ndogo ndogo ,ili aweze kusaidia  watoto wake wawili aliotelekezwa nao.

“Nawashukuru  kwa moyo wa upendo ,nitahakikisha kuwa nafuatilia maendeleo ya mwanamke huyu  tukishirikiana na Diwani mwenzangu Muna  Twalibu ,tunatamani  tumuone Magreth akiwa anafuraha na wanawake wengine kama yeye ,tutahakikisha kuwa anasimama “anasema Anna .

Kwa upande wake Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Arusha ,Wilaya ya Arumeru ,Bi Mwantumu anawaambia washiriki wa maadhimisho hayo kuwa siku ya wanawake duniani  madhumuni yake ni  kujenga ushirikiano baina ya wanawake,kutoa nafasi kwa jamii kutafakari matatizo yanayowakabili wanawake.

Mwantumu anasema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuthamini mchango wa wanawake katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi ambao awali zilikuwa hazithaminiwi kutokana na mila na desturi ambazo zilipuuza mwanamke.

Anasema kuwa chimbuko la maadhimisho hayo ni matokeo ya jitihada za umoja wa mataifa  na matokeo ya mikutano ya Kimataifa  kuhusu wanawake .

Mwaka 1935 nchi za ligi ya dunia (League of Nations)zilianza kuzungumza  haki za maswala ya wanawake kama Haki za Binadamu zinazostahili kuingizwa katika Katiba yao .

Juni mwaka 1946 Umoja wa Mataifa  ulianzisha Kamisheni  juu ya Hadhi ya Wanawake  yenye wajumbe 15.

Hata hivyo mwaka 1947 wajumbe waliongezeka na kuwa 32 ambao ni wajumbe kutoka Afrika walikuwa 8 ,kutoka Latin Amerika  wajumbe 6,Asia wajumbe 6,Ulaya Mashariki  wajumbe 6 na Ulaya Magharibi wajumbe 6.

Harakati za kumuwezesha mwanamke kuwa na haki ya kupiga kura  ulipitishwa mwaka 1952 na mwaka 1957 baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha mswada (Convention) wa malipo sawa ya Ujira  wa kazi sawa kati ya mwanamke na mwanaume.

Pia mwaka1960 mswada wa kuondoa ubaguzi wa elimu kati ya msichana na mvulana ulipitishwa na mwaka 1962 mswada wa kiwango cha umri wa kuolewa ulippitishwa .

Mwaka 1975 ,mkutani wa 1 wa wanawake  Duniani ulifanyika Mexico.Mkutano huo ulikuwa chimbuko la mwaka wa wanawake kimataifa na kuzaliwa kwa kumbukumbu ya kuzingatia usawa,maendeleo  na amani  na mfuko wa maendeleo (UNIFEM) ulianzishwa.

Mwaka 1979 mswada wa kupiga vita masuala yote ya unyanyasaji wa wanawake (Convention on the elimination of all forms of discrimination Against women) ulipitishwa  .

Mkutano wa 11 ulifanyika Copenhagen  mwaka 1980,kutathmini miaka 5 baada ya Mexico na mwaka 1985 mkutano  wa III wa Dunia  wa wanawake ulifanyika Nairobi – Kenya-Nairobi ukiwa na lengo la kubuni mikakati ya kuendeleza  wanawake kwa kuzingatia usawa wa maendeleo .

Mwaka 1995,mkutano wa IV wa wanawake ulifanyika Beijing ambalo kuzaliwa ulingo wa Beijing unao zingatia matakwa ya wanawake katika Usawa ,maendeleo  na amani

Kutokana na miswada hiyo pamoja na mikutano iliyotajwa ,mwaka 1996 ,Umoja wa mataifa uliamua maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani yafanyike tarehe 8 machi kila mwaka .

Tanzania inatambua umuhimu wa wanawake na haki zao hivyo kuwekwa wazi katika Katiba  ya Jamhuri ya mwaka 1977 .

Ibara ya 9 (g)ya katiba inasisitiza “Serikali na vyombo vyake vyote vya Umma vinatoa nafasi zilizo sawa  kwa raia wote wake kwa wanaume bila kujali rangi ,kabila ,dini ,au hali ya mtu .

Kutokana na ukweli huo Serikali iliunda Wizara maalum ya kushughulikia maendeleo ya jamii ,wanawake na watoto  kuanzia mwaka 1990 ,Wizara hiyo ndiyo inajukumu la kuratibu shughuli zote zinazohusiana na ulingo wa Beijing ndani na nje ya nchi .

Mwaka 1992 sera ya wanawake katika Maendeleo Tanzania ,ilipitishwa ,ambapo mwaka 2000,sera ya maendeleo ya wanawake  na jinsia ,ilipitishwa zote chini ya Wizara ya maendeleo ya jamii wanawake na watoto .


Mwisho………………………………………………………………………