August 24, 2015

MJUMBE WA MKUTANO CHADEMA Arumeru ,ahama na Vijana 1000 kwenda ACT Mzalendo


CHADEMA Arumeru yasambaratika ,Vijana zaidi ya 1000  wahamia ACT

Na Mary John  ,Arumeru ,Arusha

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Taifa CHADEMA  na mwenyekiti wa Kata ya Nkwandurua Wilaya ya Arumeru  Samweli   Shami  akiwa na Vijana zaidi ya 1000 wa kata ya Nkwandarua wamehamia chama cha ACT Mzalendo kwa madai ya kunyanyaswa na kunyimwa fursa  za kutumia vipaji vyao kuwaletea wananchi  maendeleo 

Mjumbe huyo akizungumza na waandishi wa habari  kwa niaba ya Vijana wenzake katika ukumbi wa Piaza Nduruma alisema kuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Joshua Nassari na Katibu wa Wilaya ,CHADEMA  wameshirikiana kuwanyanyasa Vijana wa Jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kuwanyanganya  nafasi za kuwania nafasi za udiwani 

Bw,Shami alisema kuwa  Mbunge Nassari hakubali ushindani na kuwa hataki kuona Vijana wenye uwezo wa taaluma wakiwania nafasi mbali mbali za uongozi ili wasaidie wananchi  badala yake anaweka watu kwa nguvu ,wenye kutetea maslahi yao .

Kimsingi alisema  kuwa lengo la kujiunga na CHADEMA ilikuwa ni kuweza kupata fursa ya kutumia elimu na uwezo aliyonao ili aweze  kuwaletea wananchi maendeleo 

Shamy alisema  kuwa kitendo  cha CHADEMA  Jimbo la Arumeru Mashariki kuwakata watu wenye uwezo na waliochaguliwa katika kura za maoni ni uonevu ,na kuwa hawawezi kuendelea kuona uonevu huo na kudai kuwa wananchi na wafuasi wanamuunga mkono wamebariki  ahamie chama chochote .

Alisema kuwa amehamia chama cha ACT mzalendo na kuwa anatarajia kuwa kupitia Chama hicho atawaletea wananchi maendeleo .

Pamoja  na mambo mengine  alisema kuwa wafuasi wake na wananchi wanamuunga mkono ,wameondoka  CHADEMA na kujiunga ACT mzalendo baada ya kuchukizwa na mwenendo na vitendo vinavyofanywa ndani ya chama hicho .

Fadhili mboya  Mwenyekiti wa Vijana kata ya Nkwandurua  CHADEMA  akizungumzia hatua hiyo alisema kuwa wanachukizwa na vitendo vinavyofanywa na Mbunge Nassari na kudai kuwa wanaungana na Mjumbe wa Mkutano wa Taifa CHADEMA kuhamia ACT Wazalendo 

Mboya alikiri kuwa Mbunge Nassari ameonyesha  ubabe wa wazi kwa kuwanyima watu waliochaguliwa katika kura za maoni nafasi ya kugombea nafasi za udiwani na kuwapatia watu ambao walipata kura ndogo  kitendo walichodai kuwa ni ubakaji wa demokrasia 

Lukas Kaaya ni kiongozi mwingine ambaye amenyimwa nafasi ya kuwania nafasi ya udiwani kwa kura 61 akiwashinda wenzake wanne lakini nafasi hiyo  amepatiwa  mtu ambaye aliyepata kura ndogo na kudai kuwa anahamia chama cha NCCR Mageuzi ikiwa ni kusaka haki yake ya msingi ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kaaya alisema kuwa wananchi wa Meru wanatambua uwezo wao na watawapatia kura ,na kusisitiza kuwa vitendo vya uonevu vinavyoendelea ndani ya CHADEMA Jimbo la Arumeru Mashariki vitaendelea kuvunja chama badala ya kuimarisha .

Vijana hao wamewataka wananchi kuwaunga mkono ,na kudai kuwa kuhama chama ni haki yao ya Msingi baada ya kuona matarajio waliyoyategemea hayajafikiwa .
Mwisho………………………………………………………………………………………………

No comments:

Post a Comment