May 5, 2013

Chuo cha Maendeleo jamii ,Kilichopewa kisogo na Serikali


Chuo Cha Maendeleo ya Jamii ,kilichopika wasomi wanaotumikia Taifa ,lakini kiwa kinarembwa na majengo Chakavu

NI jambo la kushangaza  kushuhudia vyuo bora na muhimu hapa nchini ,vilivyopika wasomi ambao wapo wanatumikia Taifa ,vikiwa vimepewa kisogo na Serikali ,vikiwa vinarembwa na majengo chakavu , ambao yanaondoa yanashushia chuo husika  Sifa .
Wakati umefika wa Wadau wa maendeleo kushirikiana kuboresha vyuo hivyo kwa kutambua wazi kuwa vyuo hivyo ni kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho ,kwa kuwa watoto na vijana wa kizazi kilichopo wanatarajiwa kujiunga na kusoma katika vyuo hivyo .
Serikali haina budi kuacha mkono  wa Birika ,kiasi cha kutenga bajeti kiduchu kwa  ajili ya kuendesha vyuo husika,vyuo vya Serikali vinapaswa kuboreshwa na kuwa na muonekano kama ilivyo vyuo vya watu binafsi hapa nchini ,kwa kuwa kila mtu anaamini kuwa Serikali ni bora kuliko watu taasisi  binafsi
Nalazimika kuandika makala hii baada yakuzuru baadhi ya vyuo vya Serikali Mkoa wa Arusha na kukerwa na miundo mbinu mibovu  ambayo ni majengo yaliyochoka na yalijengwa wakati wa mkoloni,.
Serikali inapaswa kuona haya ,na kutenga fedha  za kutosha mazingira bora ya wanataaluma wanakwenda kusoma katika vyuo hivyo ,ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kusoma katika mazingira bora yanayovutia na hivyo kuweza kufaulu katika masomo yao,hatimaye kumaliza na kutumikia Taifa lao.

Mpenzi msomaji miongoni mwa vyuo nilivyodhuru kuona uhalisia wa miundo mbinu ni Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kilichoanzishwa  mnamo mwaka 1963 kikifundisha kozi ya Maendeleo ya Jamii kwa ngazi ya cheti.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo hicho Anatory Bunduki ,Mnamo mwaka 1983 Chuo kilianza kufundisha na kutoa stashahada ya juu ya Maendeleo ya Jamii (Advanced Diploma) ikiwa na jumla ya wanachuo 35 na wakufunzi 15 waanzilishi.
Bunduki anasema kuwa mwaka 2003 Chuo kilipata Ithibati rasmi kutoka kwa Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE) na kuanza kutoa stashahada ya juu katika kozi mbili zingine na kufanya kozi kuwa tatu kama ambazo ni ;Usimamizi wa Program za Maendeleo ya Jamii(Management of Community Development programmes),Jinsia na Maendeleo (Gender and Development).
Nyingine ni Upangaji na uendeshaji shirikishi wa Miradi(Project Planning and Managament).
Bunduki anafafanua kuwa mwaka 2008 Chuo hicho  kilisitisha rasmi kudahili wanachuo katika ngazi ya stashahada ya juu na kuanza kutoa mafunzo katika kozi zote tatu katika ngazi ya shahada ya kwanza (Bachelors degree) na mwaka 2010/2011 Chuo kilisitisha rasmi kutoa mafunzo katika ngazi ya stashahada ya juu (phasing out) na kubaki na ngazi ya shahadaya kwanza.

Tangu kuanzishwa kwake Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Kiliwahi kuongozwa na wakuu wa Chuo wapatao nane( 8)kati ya hao wanawake wawili Bi. Florence Ghamunga 1985-1986 na Bi.Celina Shinyambala 1994-1998.

Mkuu wa Chuo wa kwanza aliitwa Captain E.P.Machumu na Mkuu wa Chuo wa sasa ni Bw. Anatory B.Bunduki.
Pamoja na changamoto Lukuki katika chuo hicho ,Bundi anasema kuwa wameweza kutoa wahitimu 2,332 katika fani zote tatu za Maendeleo ya Jamii tangu kilipoanzishwa wengi wao sasa wako kazini.
Chuo kimeweza kupanda ngazi  tofauti katika utoaji wa mafunzo ambazo ni; ngazi ya Cheti, Stashahada ya juu,  Shahada ya kwanza na Stashahada ya Uzamili.

Anaendelea kutoa historia ya chuo kuwa Chuo kinajumla ya wanachuo 543 ikiwa wanawake ni 308 na wanaume 235.Kwa upande wa wahadhiri anasema  kina jumla ya wahadhiri 27, uwiano wa mhadhiri 1 kwa wanafunzi 20.

Aidha anasema Chuo kimeweza kujitangaza kwa njia mbalimbali,  kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau mbali mbali na  kuhuisha michezo.



Katika kukabiliana na uhaba wa maji  Chuo hicho  kimefanikiwa kujenga kisima kirefu cha maji safi na salama kwa jumuiya ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii – Tengeru tangu 2003,

Hata hivyo anasema katika kuboresha miundo mbinu ya Chuo wameweza  kujenga kumbi pacha mbili za mihadhara zilizokamilika 2008, na kugharimu shs. 668,502,611.77/= zikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa wakati moja.
Bunduki anasema kuwa wanaendelea  na ujenzi wa maktaba ya kisasa unaotegemewa kugharimu jumla ya shs.513,382,914/= kwa awamu ya kwanza maktaba hii ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 kwa wakati moja.  Kumekuwepo na tatizo la ukosefu wa fedha hivyo kuchelewesha awamu ya pili ya ujenzi

Bunduki anasema kuwa wanakabiliwa na Changamoto Lukuki baadhi ya changamoto hizo zikiwa ni  Uchakavu  wa miundo mbinu ikiwa ni  madarasa, mabweni, nyumba za watumishi na jengo la utawala,na kueleza kuwa  uongozi wa Chuo unajitahidi  kufanya ukarabati wa hatua kwa hatua hususani mabweni,  zahanati, madarasa na nyumba za watumishi ikiwa ni wakati fedha zinapatikana .

Anavunja ukimya na kueleza kuwa pamoja na kujitahidi kutoa huduma wanapata vikwazo na kufanya shughuli za chuo kusuasua ,kuwa mahitaji ya uendeshaji wa Chuo mfano  mwaka  2012/2013 ni Tshs. 5,147,758,984/-lakini fedha zinazopatikana  kutokana na mapato ya ndani ni Tshs. 691,505,600/= ruzuku ni Tshs 49,583,000/=, mishahara ni Tshs. 1,121,215,924/= sawa na asilimia 36.2 tu ya mahitaji halisi ya Chuo.
Bunduki anasema kuwa  Chuo kinajitahidi kuainisha vyanzo vingine vya mapato ikiwa ni pamoja na ada za mafunzo ya muda mfupi, utafiti na ushauri wa kitaalamu.

Akizungumzia masuala mengine anasema kuwa Chuo kinakabiliwa na uhaba  wa vyombo vya usafiri  hususani pale mafunzo ya vitendo yanapohitajika  na hata katika utendaji wa majukumu ya kila siku, na kuwa Chuo  kinakabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo wahadhiri na watumishi waendeshaji. Na kufanya huduma ya taaluma kudorora .
Kwa upande wao  baadhi ya watumishi wa Chuo hicho wameeleza kuwa ,Maslahi duni yanawavunja moyo watumishi  katika utendaji wao wa kazi wa kila siku, kwa kuwa wanashindwa kumudu gharama za maisha zinazopanda kila wakati.

Watumishi hao wanasema kuwa wanaweza kukabiliana na matatizo hayo  ikiwa Serikali itatoa fursa ya chuo kujiendesha na kujisimamia chenyewe na mwongozo wa Utumishi kupitishwa.
Mkuu huyo anasema kuwa  matarajio ya badae ni Chuo ni kitahuisha mafunzo ya muda mfupi katika nyanja za uhamasishaji jamii, ubunifu na uandikaji wa miradi, uandikaji taarifa, uongozi, haki za Mama na Mtoto, Ujasiriamali n.k.  Pamoja na kutoa mafunzo ya muda mrefu chuo kinategemea pia kujikita katika ushauri wa kitaalamu na utafiti hususani katika masuala ya kijamii.Chuo kwa kushirikana na bodi ya Uendeshaji na Wizara,  kimepata ithibati ya kujiendesha kisheria katila utoaji wa mafunzo  (AUTONOMY).
Kwa upande wao Afisa habari wa Chuo hicho Clara Emanuel anasema kuwa Chuo kina mahusiano mazuri na vyuo vingine ,katika Nyanja ya michezo na mijadala ya taaluma ,na kuwa kupitia michezo wanafunzi wameweza kubadilishana uzoefu na kuepuka kujiingiza katika vitendo vya uhalifu

Anasema kuwa wanafunzi wengi katika Chuo hicho wamejikita katika taaluma zao ,na kuwa muda mwingi wanatumia kujisomea ,na kueleza kuwa nidhamu hiyo imetokana na uongozi bora wa chuo .

Kwa Upande wake mmoja wa watumishi katika maktaba ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii  Tengeru   Joseph Atanasi ,ambaye mwandishi wa makala hii alifanya mahojiano nayo anasema kuwa vitabu havitoshelezi na kueleza kuwa wanahitaji vitabu zaidi na bora vinavyoendana na wakati ,ikiwa ni kuwawezesha wanafunzi kusoma kulingana na wakati ,
Anasema kuwa vitabu vilivyo ni vya miaka ya nyuma na kueleza kuwa bado vinafaa kutumika lakini vitabu vipya vinahitajika kutokana nauhalisia wa karne hii ya Sayansi na Tekenolojia .
Tangu kuanzishwa kwake Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Kiliwahi kuongozwa na wakuu wa Chuo wapatao nane( 8)kati ya hao wanawake wawili Bi. Florence Ghamunga 1985-1986 na Bi.Celina Shinyambala 1994-1998.
Mkuu wa Chuo wa kwanza aliitwa Captain E.P.Machumu na Mkuu wa Chuo wa sasa ni Bw. Anatory B.Bunduki.
Mwisho



Serikali imekipa kisogo chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru

Jengo Pekee bora Chuo cha Maendeleo Jamii Tengeru,Serikali inatia aibu ,Chuo kina miaka 45 tangu kuanzishwa